Kampuni ya teknolojia ya Microsoft imetangaza rasmi uzinduzi wa mfumo wake mpya wa uendeshaji wa server uitwao Azure Linux 4.0, hatua inayotajwa kuwa mabadiliko makubwa katika historia ya kampuni hiyo ambayo kwa miaka mingi ilijulikana zaidi kwa mfumo wa Windows.
Tangazo hilo lilitolewa wakati wa mkutano wa teknolojia wa wazi wa Open Source Summit North America uliofanyika mjini Minneapolis nchini Marekani. Mfumo huo mpya umetengenezwa mahsusi kwa matumizi ya huduma za wingu (yaani "Clouds Services") za Azure na sasa utapatikana kwa wateja wa kawaida wa Azure kama mfumo kamili wa seva.
Azure Linux 4.0 ni nini?
Azure Linux 4.0 ni mfumo wa uendeshaji wa Linux uliotengenezwa na Microsoft kwa ajili ya seva, mashine pepe (virtual machines), mifumo ya kontena na miundombinu ya huduma za cloud. Mfumo huo unatokana na teknolojia ya Fedora Linux na umeboreshwa ili kufanya kazi kwa ufanisi ndani ya mazingira ya Azure.
Awali, Microsoft ilikuwa ikitumia mfumo huo ndani ya huduma zake za ndani chini ya jina la CBL-Mariner kabla ya kubadilishwa kuwa Azure Linux. Toleo jipya la 4.0 sasa limepanuliwa kutoka matumizi ya kontena pekee hadi kuwa mfumo kamili wa seva unaoweza kutumiwa moja kwa moja na wateja wa Azure.
Kwa nini Microsoft imeamua kuingia rasmi kwenye Linux?
Kwa mujibu wa viongozi wa Microsoft, hatua hiyo inalenga kuongeza usalama, kasi na uthabiti wa huduma za cloud huku kampuni hiyo ikiendelea kushindana katika soko la kimataifa la huduma za kompyuta za wingu.
Meneja Mkuu wa Programu za Open Source katika Azure, Lachlan Everson, alisema Azure Linux 4.0 imejengwa kutokana na uzoefu wa miaka mingi ambao Microsoft imeupata katika kutumia Linux ndani ya miundombinu yake ya Azure.
Wachambuzi wa teknolojia wanaeleza kuwa hatua hiyo pia inaonyesha namna Microsoft ilivyobadilisha msimamo wake kuhusu Linux. Miaka ya nyuma kampuni hiyo ilikuwa ikionekana kama mpinzani mkubwa wa Linux, lakini sasa imekuwa miongoni mwa kampuni zinazoongoza katika matumizi na maendeleo ya teknolojia za open source.
Vipengele muhimu vya Azure Linux 4.0
Mfumo huo mpya umepewa maboresho mbalimbali yakiwemo:
Ulinzi wa hali ya juu dhidi ya mashambulizi ya mtandao
Kernel iliyoboreshwa kwa mazingira ya Azure
Mfumo wa kisasa wa usimamizi wa paket kupitia RPM za Fedora
Uwezo wa kufanya kazi kwenye seva, kontena na mashine pepe
Ujumuishaji wa moja kwa moja na huduma za Azure
Mzunguko wa masasisho unaotabirika kwa watumiaji wa biashara
Microsoft pia imesema kuwa mfumo huo utaweza kuendeshwa kupitia Windows Subsystem for Linux kwenye Windows 11 ili kuwapa watengenezaji uwezo wa kuujaribu kwenye kompyuta zao binafsi. Hata hivyo, kampuni hiyo imesisitiza kuwa Azure Linux 4.0 haijalengwa kuwa mfumo wa desktop kwa matumizi ya kawaida ya nyumbani.
Athari kwa sekta ya teknolojia
Wataalamu wanaamini uzinduzi wa Azure Linux 4.0 utaongeza ushindani dhidi ya mifumo mingine maarufu ya Linux inayotumika kwenye cloud kama Ubuntu, Red Hat Enterprise Linux na SUSE.
Hatua hiyo pia inaonyesha namna Linux inavyoendelea kutawala katika miundombinu ya seva na cloud duniani, huku kampuni kubwa za teknolojia zikizidi kuwekeza kwenye mifumo ya open source.
Kwa sasa, Microsoft imeweka wazi kuwa Azure Linux 4.0 inalenga zaidi mazingira ya cloud na AI kuliko matumizi ya kawaida ya desktop, jambo linaloonyesha mwelekeo mpya wa kampuni hiyo katika dunia ya teknolojia za kisasa.
CHANZO: ZDNET
Microsoft Yazindua Azure Linux 4.0, Mfumo Wake wa Kwanza wa Linux kwa Server
- webmaster
- Site Admin
- Posts: 124
- Joined: Mon Mar 23, 2026 11:03 am
- Location: Pemba
- Contact:
Who is online
Users browsing this forum: No registered users and 0 guests